Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema mechi za Kimataifa za Kirafiki walizocheza zimekiimarisha kikosi chake na sasa kipo tayari kwa mapambano ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kagera Sugar iliweka kambi yake nchini Uganda na kucheza mechi kadhaa za Kimataifa za Kirafiki ikiwamo na mabingwa Vipers SC.

Kocha huyo amesema kambi hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwao ikiwemo kujenga muunganiko mzuri kwa wachezaji wake wapya na wale waliokuwepo msimu uliopita.

“Tupo tayari kwa mapambano, siwezi kusema tutakuwa mabingwa lakini lengo letu ni kupata matokeo mazuri katika kila mchezo. Natambua timu nyingine pia zimejiandaa kama sisi, kitu cha msingi tusubiri kuona matokeo ya mwisho,” amesema Maxime.

Kocha huyo amesema katika mechi hizo za kirafiki, amefurahishwa na wachezaji wapya ambao wameingia kwenye mfumo wake ndani ya muda mfupi tofauti na alivyotarajia.

Amesema hilo linampa matumaini ya kuanza vyema mechi za kwanza za ligi na kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Kagera Sugar imesajili wachezaji watano wapya ambao ni Obrey Chirwa, Ally Ng’azi, Dickson Gidion, Abiudy Mtambuku na Gasper Mwaipasi.

Mkwanja wa Rice wamuibua Roy Keane
Jeshi latoa taarifa za kuhuzunisha