Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa mwaka 2023/24 unatarajia kuanza Septemba 09 na kushirikisha jumla ya timu 16, imeelezwa.
Rais mpya wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Suleiman Jabir alisema mwishoni mwa juma lililopita jijini Dar es salaam kuwa maandalizi ya ligi hiyo yanaendelea vizuri.
Jabir au Mdau’ alisema kuwa ligi hiyo msimu huu itashirikisha timu 12 kutoka Kanda ya Unguja wakati nne zitatokea katika kisiwa cha Pemba huku timu za Ligi Daraja la Kwanza zikiwa 20 kutoka Unguja na 18 zinatoka Pemba.
Akizungumzia wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa na timu, Jabir alisema kuwa ni wachezaji tisa lakini wanaotakiwa kucheza kwa wakati mmoja ni saba.
Alisema huko nyuma klabu za Zanzibar zilibebwa na wachezaji wa nje, ambapo Malindi iliwahi kumsajili hadi aliyekuwa mchezaji bora wa Afrika, Mordon Malitoli na ilicheza nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1994.
Alisema kuwa mipango yao sasa ni kuhakikisha timu za Zanzibar zinazoshiriki mashindano ya kimataifa msimu huu zinafika mbali na sio kuishia raundi ya awali.