Wakati saa kadhaa zikisalia kabla ya Miamba ya Soka ya jijini Dar es salaam haijaumana katika Dimba na CCM Mkwakwani jijini Tanga, Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umeionya Azam FC.

Miamba hiyo itakutana leo saa moja usiku, katika mchezo wa Nusu Fainali ya kwanza ya Ngao ya Jamii, huku Young Africans ikiwa na kazi ya kutetea taji hilo wanalolimiliki kwa misimu miwili mfululizo.

Idara ya Habari na Mawasilino ya Klabu hiyo Nguli katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, imeionya Azam FC ikiiambia kama haijajiandaa vizuri na kuwa bora msimu huu, basi itarajie kukutana na kipigo kikali katika mchezo wa leo.

Mkuu wa Idara hiyo, Ali Kamwe amesema wanaitaka Azam FC iwe imejiandaa kisawasawa kwani Wanachama na Mashabiki wa Young Africans wamewaambia hawataki kitu kingine kwenye Makao Makuu ya Klabu hiyo yaliopo ‘Jangwani’ zaidi ya kurejea na Ngao ya Jamii.

“Sisi tunaiandaa timu yetu, kama hawatokuwa bora au kujiandaa vizuri tutawapa adhabu ile ile ambayo waliipata kwenye mechi ya mwisho, akili yetu ni kuijadili furaha yetu na siyo maumivu ya watu wengine,” amesema Ali Kamwe.

Mshindi wa mchezo huo wa leo atacheza Fainali ya Ngao ya Jamii 2023 dhidi ya Mshindi wa mchezo wa pili wa Nusu Fainali utakaozikutanisha Simba SC na Singida Fountain Gate kesho Alhamis (Agosti 10) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani, jijini Tanga.

Maguire amegoma Man Utd
Mashabiki wampeleka Neymar Chelsea