Kuna Hadithi moja niliwahi kuisikia kuwa Kijana mmoja alimuona Mwalimu wake aliyewahi kumfundisha Shule ya Msingi, kwenye Sherehe ya Harusi ambayo yeye alikuwa ni mwalikwa hivyo akapata shauku ya kwende kumsabahi maana, ni kitambo kilipita bila kukutana.

Kijana alienda kumsalimia kwa heshima na bashasha, akamuambia “je, unaweza kunitambua Mwalimu?’…..
‘Sidhani! naomba unikumbushe,” alijibu Mwalimu na Mwanafunzi huyo akaanza kumsimulia akisema, “nilikuwa mwanafunzi wako katika darasa la 3, na kuna siku niliiba saa ya Mwanafunzi mwenzangu kwasababu ilikuwa ya kipekee na ya kuvutia.”

“Mwanafunzi mwenzangu alikuja kwako akilia kwamba saa yake imeibwa na wewe Mwalimu ukaamuru Wanafunzi wote Darasani tusimame kwenye mstari ulionyooka, tukitazama ukuta huku mikono yetu ikiwa juu na macho yetu tuyafumbe, ili uangalie mifuko yetu,” alisema Mwanafunzi huyo.

Aliendelea kuwa, “nilianza kupata wasiwasi na hofu ya matokeo ya utafutaji ule nikiwaza aibu ambayo ningeipata baada ya Wanafunzi kugundua kuwa niliiba saa, maonia mbayo Walimu wangu wangeyapata kunihusu, kuitwa mwizi hadi niondoke Shuleni na jinsi Wazazi wangu watakavyonichukulia.”

Anasema, “wakati nikiwaza yote hayo ghafla ikafika zamu yangu ya kuchunguzwa. Nilihisi mkono wako ukiingia mfukoni mwangu, ukatoa Saa na kuweka kikaratasi mfukoni mwangu nikashikwa na hofu, nikitarajia mabaya zaidi yangetangazwa. Nilishangaa hukufanya lolote na uliendelea kupekua mifuko ya wanafunzi wengine hadi ukafika mtu wa mwisho.

Upekuzi ulipoisha, ulituomba tufumbue macho na tukae kwenye viti vyetu. Niliogopa kukaa maana nilifikiri utaniita mara baada ya kila mtu kuketi huku nikiwa na shauku ya kujua kikaratasi kile kilikuwa na ujumbe gani na kwa haraka nikakifungua kwa kificho nikakisoma “ACHA KUIBA, MUNGU HAPENDI NA NI CHUKIZO KWA WATU, UTAAIBIKA”.

Mapigo ya Moyo yalienda kasi nikibashiri kinachokuja kutokea mbeleni na kilichofuata uliionesha saa ukiwa mbele ya Darasa na ukampa mmiliki wake na hukutaja jina la aliyeiba wala hukuniambia neno lolote, na hukuwahi pia kusimulia tukio hilo kwa mtu yeyote.

Katika kipindi chote nilichokuwa shuleni, hakuna Mwalimu au Mwanafunzi aliyejua kilichotokea. Tukio hili kwa kawaida lilinifundisha somo kubwa na niliamua moyoni mwangu kamwe kutojihusisha katika kuchukua chochote ambacho si changu.

“Uliniepusha na aibu, uliniokoa na aibu pia uliilinda heshima yangu Mwalimu wangu, Je? sasa umenikumbuka, unakumbuka hadithi hii sasa Mwalimu? bila shaka huwezi kusahau kisa hiki kirahisi Mwalimu wangu, nini mimi,” alimwambia Mwalimu wake Kijana huyo.

Mwalimu akajibu, “ninakumbuka vizuri hadithi hii kwamba niliikuta Saa mfukoni lakini sikujua saa iliyoibwa ilipatikana mfukoni mwa nani siku hiyo kwa sababu nilipekua mifuko yako huku pia nikiwa nimefumba macho.” kitendo ambacho kilimshangaza kijana yule.

Hakika katika maisha, tunahitaji hekima kwa kila jambo tunalofanya kama Wazazi, Walimu, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Serikali n.k, tunapaswa kuwa na uwezo wa kufumba macho yetu kwa baadhi ya mambo kwani sio tabia zote mbaya zinahitaji adhabu.

Wengine watahitaji kutiwa moyo, wengine kushauriwa na wengine ufuatiliaji kwahiyo uwe Mwalimu au Kiongozi ama Mzazi uwe mwenye kutia moyo siku zote, sio mtu wa kuvunja moyo maana hatua unazochukua dhidi ya waliokukosea kama hadithi hii isemavyo, inaweza kubadilisha maisha na tabia za wakosaji.

Mazingira Hospitali ya Dodoma yawavuta Wanandoa
Kevin de Bruyne awekewa mtego Saudi Arabia