Uongozi wa Young Africans umewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wake kufuatia taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kuhusu vibali vya Wachezaji wa Kimataifa wa klabu hiyo.

Mapama leo Jumatano (Agosti 09) TFF ilitoa taarifa za kutopokea vibali vya Wachezaji wa Kimataifa wa Simba SC, Young Africans na Singida Big Stars, hivyo hawataruhusiwa kucheza michezo ya Ngao ya Jamii na Ligi Kuu.

Afisa habari wa Young Africans Ally Kamwe amesema Wanachama na Mashabiki wao wanapaswa kuwa na amani, kwa sababu taratibu zote kuhusu vibali vya wachezaji wao wa Kimataifa zimeshakamilisha na kuwasilishwa TFF.

Kamwe amesema wameona taarifa iliyotolewa na TFF, lakini Uongozi wa Young Africans tayari ulikuwa umeshakamilisha taratibu zote, hivyo wana uhakika Wachezaji wao wa Kimataifa wataruhusiwa kuchezwa dhidi ya Azam FC baadae leo Jumatano (Agosti 09).

“Tumeona taarifa yao na hadi muda huu tumeshakamilisha vigezo vyote vya wachezaji wetu ambao tumewasajili msimu huu. Hivyo Wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wowote ule” amesema Ally kamwe kupitia Yanga TV

Ikumbukwe kuwa Michuano ya Ngao ya Jamii inaanza rasmi leo Jumatano (Agosti 09) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga, ambapo Mabingwa watetezi Young Africans watapapatuana na Azam FC, huku Simba SC ikitarajiwa kupambana na Singida Fountain Gate kesho Alhamis (Agosti 10).

TFF yaukubali mziki Young Africans
Azam FC yazipiga bao Simba, Young Africans