Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdi-hamid Moalini, amesema ameridhishwa na utimamu wa mwili kwa wachezaji wake lakini anaendelea kuwasoma wapinzani wao Young Africans kuekelea mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 15, mwaka huu.

KMC itacheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya bingwa mtetezi, Young Africans, Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Moaiini, amesema anatumia siku chache zilizosalia kwa ajili ya kutengeneza muunganiko wa wachezaji wake kabla ya kukutana na mabingwa hao watetezi katika mchezo huo wa kwanza.

Moalini amesema kikosi chake kilifanya mazoezi mbalimbali ikiwamo ya utimamu wa mwili, mbinu za ufundi kwa muda wa majuma matatu, jambo ambalo limeimarisha wachezaji wake.

Kocha huyo raia wa Marekani mwenye asili ya Somalia amesema kazi kubwa aliyonayo sasa ni kuhakikisha nyota wake wanakuwa na muunganiko kwa sababu ya uwepo wa wachezaji wapya na zamani.

“Maendeleo ni mazuri, tumetumia vizuri majuma mawili ya maandalizi ya msimu mpya, kwa ajili ya kujenga utimamu wa mwili, sasa bado nafanyia kazi muunganiko, naamini muda wa siku saba zilizobakia tutazitumia vizuri ili kupata matokeo chanya dhidi ya Young Africans,” amesema kocha huyo.

Wakati huo huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, amesema baada ya kukamilisha usajili, timu yao iliweka kambi ya muda mrefu mkoani Morogoro.

“Sasa ninavyozungumza tayari kikosi kipo Dar es salaam kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Young Africans.

Kocha Moalini bado ni mgeni lakini tumempa muda kidogo wa kutengeneza timu yake,” amesema ofisa huyo.

Chelsea yamfikiria Dusan Vlahovic
Nkunku kuwa mtazamaji Chelsea