Wawakilishi wa Visiwani Zanzibar katika Michuano ya Kimataifa kwa klabu msimu huu 2023/24, Kikosi Maalunu cha Kuzuia Magendo (KMKM) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) watacheza mechi zao kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, jijini Dar es salaam.
Rais wa Shirikisho la Soka visiwani Zanzibar ‘ZFF’, Suleiman Jabir amesema kuwa timu hizo zitachezea Chamazi Conplex kama uwanja wao wa nyumbani baada ya ule wa Amaan Zanzibar kuwa katika ukarabati mkubwa.
KMKM itaiwakilisha Zanzibar katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa wakati JKU wenyewe watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Jabir alikiri kuwa timu za Zanzibar zimekuwa hazifanyi vizuri katika mashindano ya CAF, lakini aliahidi kuwa mwaka huu wanataka zifike mbali na ndio maana zimeanza maandalizi mapema.
KMKM itaanza kampeni ya kusaka Ubingwa wa Afrika (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika) hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya St. George ya Ethiopia katika mchezo utakaopigwa Chamazi kati ya Agosti 18, 19 na 20 wakati JKU wataanza dhidi ya Singida Fountain Gate.