Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino wa Azam FC, Thabiti Zakaria ameeleza kuwa pamoja na kiwango alichokionesha Mlinda Lango wao, Zuberi Foba kwenye mechi yao dhidi ya Young Africans lakini anapaswa kupewa nafasi ya kuzidi kuimarika.

Akitolea mifano ya Aishi Manula, Farid Mussa na Bakari Kimwaga miongoni mwa wachezaji wanaowika nchini alifafanua mechi zao za kwanza wakati wapo Azam FC waliumana na Young Africans lakini kila mmoja anafahamu ubora wao kwa sasa.

“Aishi Manula (anayekipiga Simba) ambaye leo ni Tanzania One mechi yake ya kwanza ilikuwa ya Ngao dhidi ya Young Africans mwaka 2013 na tulifungwa, Farid Mussa (sasa yupo Young Africans), Bakari Kimwaga hawa walianzia mechi zao za kwanza wakicheza na Young Africans, ni mechi kubwa kwao lakini leo wanafahamika vizuri.

“Kwa hiyo suala isiwe Foba sana kwa maana wachezaji lazima wacheze ndio wakue na wachezaji wengine wanaanza kwenye mechi kubwa sana, anaweza akaanza hata kwenye Fainali ya Ligi ya Mabingwa, hivyo isiwe kitu kikubwa sana,” alisema Zakaria.

Amesema hata mashabiki wanaouliza juu ya kiwango cha kipa huyo wanapaswa kufahamu ili chuma kiwe cha pua lazima kipite kwenye moto mkali kwa maana ya mechi nzito zinamjenga mchezaji ndio maana Foba akapewa nafasi.

Kipa huyo aliyeibuka kwenye timu ya vijana ya Azam FC, amekuwa gumzo kwenye mechi ya juzi Jumatano (Agosti 09) ya Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans waliyofungwa mabao 2-0 Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga akikosolewa kwa kiwango hafifu alichokĂ­onesha.

DAWASA yajenga mitambo ya kuchakata Majitaka
Kylian Mbappe kukosa mchezo wa ufunguzi