Baraza la Taifa la uwezeshaji Wananchi – NEEC, limejipanga kuendeleza makubaliano na Chuo cha Usimamizi wa Fedha – IFM, ili kuwajengea uwezo wananchi katika masuala ya usimamizi wa fedha na kuleta tija katika masuala ya kiuchumi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Agosti 14, 2023 jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa amesema wananchi wanapaswa kujua namna ya kusimamia uchumi wao binafsi, hivyo hawatochoka kuwajengea uwezo.

Amesema, “Baraza litaboresha mfumo wa uratibu kidigitali wa ukusanyaji na uchakataji taarifa ili kutoa ripoti ya kitaifa  pamoja na kutekeleza programu ya kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika manunuzi ya umma kwa kuendesha mafunzo maalum jinsi ya kutumia mifumo mbalimbali ya manunuzi.”

Aidha ameongeza kuwa Baraza hilo pia litaendeleza na kumaliza urasimishaji wa biashara za wanawake na vijana nchi nzima.

“Na hii itasaidia wafanyabiashara kupata mikopo na mafunzo ya biashara kwa urahisi zaidi Nchini pamoja na Kuunganisha mifuko ya uwezeshaji katika utoaji wa mikopo na dhamana katika taasisi za kifedha zinazotoa mikopo.” amesema Issa.

Hata hivyo, ameongezea wataendelea kuboresha vikundi vyote vya kifedha nchini kama vile VICOBA, kwa kuvishauri, kuvihamasisha na kutatua changamoto zao ili vikue.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 15, 2023
Kambi upimaji Afya, matibabu kuzinduliwa Tanga