Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Brazil Neymar da Silva Santos Júnior ameamua kuachana na maisha jijini Paris, Ufaransa na kutimkia zake Saudia Arabia ambako anakwenda kulipwa kibosi zaidi.

Nyota huyo ameafikiana na Al-Hilal na jana jioni ilitarajiwa dili lake la Euro 160 milioni kwa miaka miwili linakwenda kumpa mkwanja wa maana zaidi katika masiha yake.

Kwa mujibu wa L’Equipe, PSG na timu hiyo ya Saudi Pro League wamefikiana makubaliano ya uhamisho wa Neymar, huku mwandishi mahiri Julien Laurens akiripoti kuwa Les Parisiens watapokea ada ya Euro 90 Milioni, huku muhusika akikubali mkataba wa miaka miwili.

Neymar mwenye umri wa miaka 31 alikuwa nje ya uwanja tangu Machi, mwaka huu kufuatia upasuaji wa kifundo cha mguu wa kulia ili kutatua changamoto za majeraha yanayomsumbua tangu alipohamia PSG kwa rekodi ya dunia kutoka FC Barcelona 2017 iliyogharimu Pauni 196 Milioni.

Licha ya kufunga mabao 118 akiwa PSG, Neymar amekuwa na uhusiano mbaya na Mashabiki wa klabu hiyo katika siku za karibuni waliowahi kuandamana nje ya nyumba mwaka huu.

Msimu huu aliambiwa pamoja na Marco Verratti watafute timu mpya kama hawataki kuendelea kukipiga kwa miamba hiyo ya jijini Paris.

Yafahamu maeneo matano ya kuogofya zaidi Duniani
Yacouba Sogne atoa mkono wa kwaheri