Baada ya kuirejeshea heshima Simba SC ya kutwaa Ngao ya Jamii Kocha Mkuu wa klabu hiyo Roberto Oliveira Robertinho ametuma salamu ya vitisho kwa watani wao Young Africans akiwaambia Ngao ya jamii imetangulia tu, lakini dhamira yake kubwa ni kuwapoka mataji mengine ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho TZ Bara ‘ASFC’.

Kocha huyo amesema hatua ya kwanza imekamilika kwa kulichukua taji hilo na sasa inakuja opresheni nyingine kabambe na wamedhamiria kubeba makombe yote.

Robertinho amesema ingawa haikuwa rahisi kuchukua taji hilo lakini kikosi chake kinataka kutumia Morali hiyo kuanza kukimbia haraka kwenye ligi ikiwa ni hatua ya hesabu ya kuchukua mataji mengine.

“Haikuwa rahisi lakini nawapongeza wachezaji wangu hii ni mechi ya watani huwa ina ugumu wake lakini kwetu jambo kubwa tumechukua hili tají la kwanza na sadfari inayofuata ni kuanza kuyasaka mataji mengine” amesema.

“Unapoanza msimu na mafanikio kama haya kuna morali kubwa inajengeka kwenye mioyo yetu, nimekuta klabu hii ina miaka miwili bila taji, kwa hadhi ya Simba haikuwa sawa sasa tunaingia kwenye ligi tukiwa na nguvu kubwa.

“Mimi ni kocha ambaye kote nilikopita nimekuwa natamani kuchukua mataji na nimekuwa nayapata, bahati mbaya hapa mwaka wa kwanza sikupata kombe lolote na kulikuwa na sababu na huu ni mwanzo.

Robertinho amekiri kuwa kikosi chake hakikucheza vizuri kwenye mchezo huo hasa kipindi cha kwanza akiutaja uwanja kwamba uliwazuia kucheza mpira wao wa Samba lakini pia muunganiko wa wachezaji wake haukuwa mzuri.

“Nimeona watu wanasema hawajafurahi, ni kweli najua mashabiki wa Simba wanataka kuiona timu yao inacheza mchezo wa kuvutia lakini ilikuwa ngumu kucheza soka la aina ile kwenye uwanja wa namna ile.

“Hatukucheza vizuri kweli kipindi cha kwanza nikasema kipindi cha pili tubadilike kutoka ule mfumo wa 4-2-3-1 kuja 4-3-3 ambao kwa kiasi ulitufanya ulitufanya tuwadhibiti wapinzani wetu.

“Kila kitu kinakwenda kwa nafasi yake, kwa uwanja ule kitu cha kwanza na bora ilikuwa kuchukua taji lakini sasa tunarudi kuendelea kuwaunganisha wachezaji, nilisema tunahitaji siku zisipungua kumi na tano kuanza kuona Simba iliyokamilika na kucheza kama tunavyotaka.”

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 16, 2023
Hii hapa mikakati ya Simba SC 2023/24