Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema huenda kuna Baadhi ya Mabalozi wa Tanzania hawajui wanachotakiwa kukifanya kwenye vituo vyao vya kazi, na kwamba wengi wao huonekana kwenye matukio pekee.

Rais Samia ameyasema hayo hii leo Agosti 16, 2023 baada ya kuwaapisha Mabalozi Wateule Ikulu Chamwino, jijini Dodoma na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia mahitaji ya nchi na mwelekeo wa Dunia kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiulinzi na kiusalama na si kuwa kama chama cha siasa kisicho na dira na kinachoendeshwa na matukio.

Amesema, “hatuwezi kufanya kazi peke yetu, tunahitaji wenzetu na sisi tunahitajika kwa wenzetu, tunakwenda katika nchi hizo kuwakilisha taifa letu kwao, mambo mtakayoyafanya au maneno mtakayoyasema kule huo ndio msimamo wa Rais na taifa letu, ukifanya kinyume hayo ni yako, matendo yako yatalifaidisha taifa au yatalifedhehesha.”

Aidha, Dkt. Samia ameongeza kuwa, “mahitaji yetu na siasa za kikanda ulimwenguni ndio zinazoamua mwelekeo wa diplomasia yetu, bila kuzingatia haya ni sawa na kuwa na chama cha siasa kisichokuwa na dira wala ajenda, kuna tukio limetokea ndio linadakwa hilohilo, sasa sisi kama mabalozi hatuendi hivyo, tunakwenda tukiwa tunajua mwelekeo wetu kama Tanzania ni kitu gani.”

Serikali yapanga kutekeleza miradi mikubwa ya Maji
Serikali yashauriwa uwezeshaji Vijana kiuchumi