Jeshi la Polisi Mkoani Tanga, linawashikiliwa watu wawili kwa makosa tofauti ya ya mauaji akiwemo Swalehe Miraji Ally (38), anayetuhumiwa kuwauwa mkewe na shemeji yake na mtuhumiwa Rajab Athuman (32), anayedaiwa kumuuwa kwa kumkata kichwa mtu mmoja, Helena Sila.

Kwa mujibu wa taarifa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi amesema Miraji ambaye ni fundi Ujenzi mkazi wa Mkanyageni Wilayani Muheza, aliwauwa Mwanahawa Hassan (24), na Sauda Sufian (20) kwa kuwakata kwa mapanga kichwani wakiwa shambani na kisha kukimbilia Mkoani Tabora.

Katika tukio jingine, Kamanda Mchunguzi amesema jeshi hilo pia limewatia hatiani watu watano kwa makosa mbalimbali akiwemo Ally Kilulu aliyehukumiwa miaka 15 jela kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin gram 1, Amos Hamis aliyehukumiwa miaka 14 jela kwa kubaka huku Halid Yusufu akihukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la wizi wa mifugo.

Wengine ni Bakari Mohammed aliyehukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la kuvunja Duka usiku na kuiba, Ernest Petro akihukumiwa miaka 20 jela kwa kosa la kuzini na ndugu yake, huku akiwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Kamanda Mchunguzi amesema, “Wananchi wa mkoa wa Tanga muendelee kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika maendeo yenu na kutumia wakaguzi kata wa Jeshi la Polisi waliopo katika kata zote kuzuia viashiria vya uhalifu na wahalifu kabla haujatendeka katika maeneo yenu.”

TAKUKURU yabaini madudu risiti za EFD
Young Africans kulipa kisasi Ligi Kuu