Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara ‘TPLB’, Almas Kasongo amesema bodi hiyo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, hawahusiki katika sakata la timu ya Kitayosce kushindwa kutumia wachezaji wake wapya iliyowasajili kwenye dirisha kubwa msimu huu bali ni uzembe wa viongozi wa timu hiyo.
Juzi Jumatano (Agosti 16) timu hiyo ilijikuta ikicheza pungufu na wachezaji wanane uwanjani katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC na kufungwa mabao 4-0 kabla mchezo huo haujavunjika baada ya wachezaji wawili wa timu hiyo akiwemo kipa kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo huo kwa mujibu wa kanuni.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kasongo amesema awali timu hiyo ilifungiwa kufanya usajili na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ baada ya kupitisha siku 45 bila kumlipa mchezaji ambaye alikwenda kuwashitaki wakati wakiwa wanashiriki ligi ya Championship msimu uliopita.
“Adhabu ya FIFA haihusiani na hiki ambacho viongozi wa Kitayosce wamekifanya, viongozi wameshindwa kuwalipia vibali vya kufanya kazi nchini wachezaji 12 wa kigeni lakini Bodi ya Ligi, TFF wala hawahusiki katika hilo, wazembe ni viongozi sababu sisi kama Bodi ya Ligi tangu asubuhi ya siku ya mchezo tulikuwa tunawauliza na majibu yao yalikuwa tumekamilisha kila kitu,” amesema Kasongo
Kwa upande wao Kitayosce kupitia Ofisa Habari wao, Pendo Lema amesema walifuata taratibu zote kwa kuwalipia wachezaji wao vibali TFF na kuambiwa mtandao unasumbua hivyo wasubiri majina ya wachezaji wao yaingizwe.