Serikali Mkoani Kilimanjaro, imesema itagharamia msiba wa watu 10, waliopoteza maisha katika eneo la Dachikona, Kijiji cha Wiri, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, baada ya gari la Polisi kugongana na gari dogo la mizigo maarufu kama Kirikuu.
Hatua hiyo imefikiwa bada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu baada kumtembelea majeruhi mmoja aliyenusurika katika ajali hiyo, ambaye amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Siha.
Amesema katika ajali hiyo, waliofariki sita ni wanawake na wanne ni wanaume akiwemo Askari Polisi ambaye alikuwa ni dereva wa Lori hilo na majeruhi huyo mmoja na kwamba watu hao waliokuwa kwenye Kirikuu walikuwa wakielekea katika mnada wa mifugo wa Ngarenairobi.
Aidha, Babu alisema chanzo cha ajali hiyo ni gari la Kirikuu kupasuka tairi na kisha kukosa mwelekeo hali iliyopelekea kugongana na lori la Polisi ambalo nalo lilikosa mwelekeo na kwenda kugonga mti huku akiitaka amii kutambua kuwa magari aina ya kirikuu, pick-up na malori si ya kubeba abiria.