Uongozi wa Klabu ya KMKM ya Zanzibar, umesema kukosekana kwa wachezaji wao wanne wa kigeni kutokana na kutokamilika kwa vibali vyao vya uhamisho wa Kimataifa (ITC), ndicho kilichoigharimu timu yao na kupoteza mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. George ya Ethiopia, lakini tatizo hilo kwa sasa wamelitatua jambo linalowapa matumaini kuelekea mechi ya mkondo wa pili utakaopigwa  ugenini mwishoni mwa juma hili.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanjwa wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, KMKM ilikubali kipigo cha mabao 2-1, hivyo inapaswa kwenda kupindua meza katika mechi ya marudiano Ethiopia ili kusonga mbele.

Naibu Katibu Mkuu wa KMKM, Suleiman Rajabu, alisema changamoto hiyo ilichangia kuvuruga malengo ya benchi la ufundi, hivyo kulazimika kutumnia wachezaji wengine.

Alisema taratibu za kukamilisha vibali vya wachezaji hao zinaendelea vema na kuweka wazi mpaka kufikia kucheza mchezo wa marudiano nchini Ethiopia Agosti 27, mwaka huu vitakuwa tayari.

“Kukosekana kwa wachezaji wetu hao kumechangia kwa kiasi kikubwa tuanze vibaya mashindano hayo, naamini mpaka ifike Agosti 27 katika mchezo wa marudiano kila kitu kitakaa sawa,” alisema Rajabu.

Alisema kikosi chao kitaendelea kubaki jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta mchezo mmoja wa kirafiki ili kuwaweka kuelekea nchini Ethiopia Ijumaa (Agosti 25).

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa KMKM Masoud Djuma, alisema bado ana kazi kubwa ya kufanya kwenye safu yake ya ushambuliaji kuelekea mechi ya mkondo wa pili.

Akizungumza jijini Dar es salaam Masoud alitaja mambo mawili ambayo yaliyowaangusha kwenye mechi ya kwanza kwamba ni kushindwa kutumia nafasi nyingi walizozitengeneza pamoja na wachezaji wake kukosa uzoefu kwenye michuano ya kimataifa.

Alisema suala la ushambuliaji analifanyia kazi ili kuhakikisha wachezaji alionao wanaweza kumpa kitu katika mchezo wa marudiano.

“Tunawakosa washambuliaji wanne hawana vibali (ITC), tumelazimika kubadilisha baadhi ya wachezaji kuwa wafungaji, naifanyia kazi safu hiyo kwa kuwaongezea mbinu ili kupata matokeo mazuri mechi yetu ya mkondo wa pili.

“Naamini haitakuwa mechi rahisi, ila nina imani kubwa na wachezaji wangu kubadilisha matokeo dhidi ya St George, hii ni kutokana na mechi ya juzi kipindi cha pili kucheza vizuri na kutawala mchezo,” amesema Masoud.

Guardiola afichuwa alichomwambia shabiki
Erik ten Hag aanza kujitetea Man Utd