Haruna Juma – Rukwa.

Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa – TAKUKURU, Mkoa wa Katavi imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi Watumishi saba kwa tuhuma za wizi wa Tsh. Bilioni 1.23 kwa kudanganya kuwa walikuwa wakilipa wakandarasi waliofanya kazi katika Halmashauri ya Mpimbwe.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5/2023 imetajwa mbele ya hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Gway Sumaye na Mwendesha mashtaka, Gregory Mhangwa ambapo amesema watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kujihusisha na genge la uhalifu, uhujumu uchumi na shitaka la tatu ni wizi.

Mhangwa ameeleza kuwa washitakiwa hao walishirikiana kutenda makosa hayo kati ya Novemba 1, 2022 hadi Agosti 11, 2023 huko katika Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe.

Waliopandishwa kortini leo ni Canuthe Hipolite Matsindiko (41) ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Michael Mathew Katanga (31) Mhasibu wa Halmashauri ya Mpimbwe, Tamaini Richard Misese (47) aliyekuwa Afisa TEHAMA mkoa wa Katavi na Maira Samson Olumba (38) Afisa Manunuzi wa Halmashauri ya Mpimbwe.

Wengine ni Emmanuel Damas Saranga (37) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe, Masami Andrew Mashauri (49) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe na Laurent William Sunga (33) Mhasibu katika Halmashauri ya Mpimbwe.

Washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na wamerudishwa rumande hadi Septemba 4, 2023 kesi hiyo itakapotajwa tena katika Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga.

Liverpool inajiamini kwa Gravenberch
ECOWAS yakataa pendekezo la watawala wa Kijeshi Niger