Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kujengea tabia ya kupima afya mara kwa mara badala ya kusubiri hadi waugue, kwani upimaji utasaidia kuepuka gharama kubwa za matibabu, kwani baadhi ya watu wamekuwa hawapimi afya zao kwa muda mrefu.

Akizungumza katika ufunguzi wa kambi ya upimaji afya itakayochukua siku tano jijini Tanga hii leo Agosti 22, 2023, Waziri Ummy amesema, mazoea hayo ni mabaya kwani yamewasababishia watu wengi matatizo ya kutopata matibabu yanayostahili na yenye gharama.

Amesema, “wengine tumezoea kula vyakula vyenye mafuta mengi tukiamini hicho ndicho chakula bora kumbe tunajichimbia wenyewe kaburi la kifo kutokana na kuzidisha mafuta ambayo ndiyo kisababishi cha madhara ya afya yetu ulaji wa baadhi ya vyakula unaweza ukawa ni sababu ya kupata maradhi.”

Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, pia amewataka Watanzania kufanya mazoezi ya miili ikiwa pamoja na kutembea, kukimbia au hata kuzunguka nyumba unayoishi mara kadhaa ili mradi watokwe na jasho, na kuwasisitiza uepukaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi.

Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi ya AfyaCheck, Dkt. Isack Maro alisema katika siku tano watakazoendesha zoezi hilo, mkazo mkubwa utawekwa katika magonjwa yasiyoambukiza, ambayo ni pamoja na yale ya msukumo (Pressure), na Kisukari.

Amesema, amevutiwa na mwitikio wa watu katika zoezi hilo kwani makisio ya awali ilikuwa angalau watu 400 wangehusika, lakini waliojiorodhesha wamefikia watu 1400 hali inayoonesha kuwa huenda idadi ya watu watakaohudumiwa wakafikia zaidi ya 5,000.

Kocha Azam FC ataja sababu za kichapo
Joao Cancelo akaribia FC Barcelona