Siku chache baada ya Rais Samia kutengua uteuzi wa Nadhifa Kemikimba kama Katibu Mkuu Wizara ya Maji, kinachodaiwa kumponza kimewekwa wazi mitandaoni.

Taarifa ya kutenguliwa kwenye wadhifa huo, ilitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus ambapo haikueleza sababu za kutenguliwa.

kipande cha video cha dakika 4:13 kinachosambaa kwa mitandaoni kikionyesha tukio la Agosti 4 mwaka huu linalomuhusisha Kemikimba, kinadaiwa kuwa huenda ikawa ndiyo sababu.

Kipande hicho kilichorekodiwa wakati wa kikao kazi cha cha kufungua mwaka mpya wa fedha cha wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Kemikimba alionekana akihamaki baada ya kupelekewa kikaratasi wakati akizungumza na kumtaka ahitimishe hotuba yake, jambo ambalo hakulikubali.

Mara baada ya kupokea kikaratasi hicho kilichotoka mbele ya meza kuu, alikisoma kisha akakitupa ilipokuwa meza kuu yenye viongozi mbalimbali akiwemo mgeni rasmi, Waziri wa Maji na Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa, Jenerali mstaafu, Davis Mwamnyange.

Na kusikika akisema kuwa “Nyinyi watu wa Human Resource (rasilimali watu) mfanye kazi yetu, haiwezekani mimi naongea hapa, mtu ananiletea kinote na kama ingekuwa hivyo msingetuita, mngefanya kikao chenu wenyewe.

“Mimi sipendi insubordination (dharau), sipendi insubordination. Mimi natoa maagizo ya sekta…Mheshimiwa waziri (Aweso) nakuheshimu wewe, namheshimu mwenyekiti wa bodi, otherwise (vinginevyo) ningeondoka, siwezi,” alisema Kemikimba.

Katika kipande hicho cha video,  kinamwonyesha Waziri Aweso akijaribu kumsihi Kemikimba awasamehe watendaji ‘walimkosea’ kwa sababu yeye ndiye katibu mkuu wao na kwamba kama kiongozi anatakiwa kuwa na ngozi ngumu.

Rais Samia aridhia ufufuaji kituo mafunzo ya Kilimo
Mikopo kausha damu yamuibua RC Manyara