Uongozi wa Simba SC umesema kuwa unafahamu kwamba timu hiyo haichezi katika ubora wake lakini unaamini hilo ni suala la muda na Kocha wao Roberto Oliveira Robertinho ataliweka sawa muda si mrefu na Wanasimba watafurahi.

Hayo yameelezwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally baada ya kuwepo kwa manung’uniko kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo wakihitaji kuona kiwango cha kuvutia katika mechi zao ingawa timu inapata ushindi.

“Ni kweli bado hatujafikia kile kilele cha ubora wetu kama Simba SC lakini zipo sababu nyingi za msingi, mojawapo ikiwa ni ugeni wa wachezaji wengi, wachezaji 11 wote wapya na sio rahisi kwa idadi hiyo kwa muda mfupi wakazoeana na kucheza vizuri kitimu.

“Lakini tunalipongeza Benchi la Ufundi chini ya kocha Robertinho na wasaidizi wake na wachezaji kwa kazi kubwa, ni muda mfupi lakini wamepambana kuipigania Simba SC na sasa tuna pointi na mabao sita,” amesema Ally.

Meneja huyo amefafanua kuwa kinachohitajika sasa kwa timu hiyo ili kuendeleza ushindi ni umoja baina ya mashabiki, Benchi la Ufundi, Wachezaji, Viongozi akiamini hakuna kinachoshindikana kwenye Nguvu Moja kama ilivyo kauli yao mbiu.

Simba SC ambao ni mabingwa wa Ngao ya Jamii 2023, imeshinda mechi zake mbili za awali za Ligi Kuu Bara, ikiifumua Mtibwa Sugar mabao 4-2 kabla ya kuichapa Dodoma Jiji mabao 2-0 na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 24, 2023
Kaze: Namungo FC itakuwa bora Ligi Kuu