Kiungo Mshambuliaji ‘Winga’ mpya aliyesajiliwa Manchester City, Jeremy Doku, amefunguka kuwa angekuwa na maisha tofauti isingekuwa ushauri wa nyota wa zamani wa Liverpool, Sadio Mane.
Winga huyo alifikiria kujiunga na Liverpool miaka mitano iliyopita wakati anakipiga Anderlecht mwaka 2018, lakini kauli ya Mane ilimkatisha tamaa.
Doku mwenye umri wa miaka 21, aliweka wazi kwamba aliwahi kupewa jezi ya Mohamed Salah kama zawadi na endapo dili hilo lingekamilika Liverpool ingelazimika kulipa Pauni 500,000 ukilinganilisha na Pauni 55 Milioni ambazo Man City imetoa kumnasa.
Lakini uhamisho huo haukufanyika na ametoboa siri kwamba alizungumza na Mane aliyemwambia muda wa kufanya uamuzi mkubwa katika historia ya soka lake ulikuwa bado.
Akizungumza na mwaandishi wa habari wa Ouest France kuhusu mipango ya kuhamia Liverpool mwaka 2018 alisema: “Nilikuwa bado mdogo nilikuwa na umri wa miaka 16, timu nyingi zilikuja na kuonyesha nia ya kunisajili, Liverpool ndio walivutiwa zaidi, Arsenal na Chelsea zilikuwepo pia.
“Nakumbuka nilienda kufanya ziara Liverpool na wazazi wangu, tulionyeshwa maeneo ya uwanja wa Anfield, pia walinipa jezi ya Salah iliyosainiwa na nikakutana na wachezaji.
“Niliongea na wachezaji wengi kama Simon Mignolet kwa sababu alikuwa Mbelgiji, Georginio Wijnaldum kutoka Uholanzi.
Pia nilizungumza sana na Mane lakini hatukuzungumza kuhusu soka tulizungumza mambo tofauti. Aliniambia nilikuwa mdogo bado ni muda mwingi na hakunishawishi kujiunga na Liverpool aliniambia tu utafanikiwa siku moja.”