Saa chache zikisalia kabla ya kushuka dimbani katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Bahir Dar ya Ethiopia, Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema kikosi chake kimejipanga vizuri kuhakikisha wanapindua meza kibabe.

Azam watawakaribisha Bahir Dar katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaochezwa leo Ijumaa (Agosti 25) katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam majira ya saa 1:00 usiku.

Katika mchezo wa kwanza Azam ilikubali kichapo cha mabao 2-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa Abebe Bikila mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atapambana na Club Africain ya Tunisia kuwania kuingia hatua ya makundi.

Akizungumza jjini Dar es Salaam, Kocha Dabo amesema amekipanga vyema kikosi chake kuhakikisha hawapotezi mchezo huo katika uwanja wake wa nyumbani.

“Tunahitaji kupindua meza na hilo linawezekana kwani nimekijenga kikosi changu vizuri na kurekebisha mapungufu yote yaliojitokeza katika mchezo uliopita na sasa tupo tayari kuhakikisha tunashinda mchezo huo muhimu,” amesema Dabo.

Nyota wa timu hiyo, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’, amesema wamejipanga vizuri kuelekea mchezo huo muhimu na kikubwa wanahitaji ushindi na kuendelea kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa.

Fei Toto amesema kama wachezaji watahakikisha wanafuata maelekezo yote waliyopewa na benchi lao la ufundi kuweza kupata ushindi wa mabao mengi.

“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapindua meza, kubwa tunacheza katika uwanja wetu wa nyumbani hivyo tutatumia vyema uwanja huo kwa kuwaadhibu wapinzani wetu,” amesema Fei Toto.

Hata hivyo, Fei Toto amewaomba mashabiki na wapenzi wa timu yao kuhakikisha wanajaa kwa wingi uwanjani kuweza kuwapa sapoti kwani sapoti yao ndio itawasaidia kupata ushindi.

Wapongezwa kwa kutumia vyema nafasi za Ubunge
Joao Cancelo ni suala la muda tu!