Mkuu wa SADC, Nevers Mumba ameukosoa Uchaguzi wa Zimbabwe akisema ujumbe wake umebaini baadhi ya vipengele vina mapungufu kulingana na katiba ya Taifa hilo, sheria ya uchaguzi na misingi ya SADC ikiwemo miongozo inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia.
Hatua hiyo, inakuja baada ya Waangalizi wa uchaguzi kutoka jumuiya ya kikanda ya kusini mwa Afrika – SADC, kusema uchaguzi wa rais na wabunge nchini Zimbabwe haukufuata misingi ya kidemokrasia na uwepo wa ukandamizaji.
Ujumbe huo, unasema pia ulibaini kuwa awamu za kabla ya uchaguzi na upigaji kura, zilikuwa na amani na utulivu lakini kufutwa kwa mikutano ya upinzani na shutuma za kunyanyaswa kwa wapiga kura ni miongoni mwa baadhi ya masuala yaliyovuruga uchaguzi.
Uchaguzi huo, unaangaliwa kote kusini mwa Afrika kama mtihani wa uungaji mkono kwa chama cha Rais Emmerson Mnangagwa cha ZANU-PF, ambacho utawala wake wa miaka 43 umekumbwa na mdororo wa uchumi ulioporomoka na uwepo wa utawala wa kimabavu.