Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka Wakurugenzi wa Huduma kwa wateja wa Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha wanayasimamia majukumu yao ya kimsingi pamoja na kutoa huduma bila upendeleo, ikiwemo kutoa taarifa sahihi na kwa lugha inayoeleweka kirahisi, Kushirikisha wateja na wadau mbalimbali katika kuboresha utoaji wa huduma.
Aweso ameyasema hayo wakati wa kikao kazi na kufunga Kikao Kazi cha Wakurugenzi wa Huduma kwa wateja wa Mamlaka za Maji na kuongeza kuwa pia wanatakiwa kujenga mahusiano mazuri na wateja, Kupokea, kusikiliza na kushughulikia masuala yote yanayoletwa na wateja.
Amesema pia Viongozi hao wanatakiwa kutoa elimu kwa wateja kuhusu huduma zitolewazo na Mamlaka, kuwashirikisha wateja wakati wa usomaji wa dira na uandaaji wa ankara za maji, kuhakikisha kuwa huduma ya maji inakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kutunza vyanzo vya maji.
Aidha, Aweso ameongeza kuwa, jukumu jingine ni kuzingatia kanuni zote za uendeshaji wa Mamlaka za maji ikiwa ni pamoja na kutowakatia wateja huduma ya maji siku za sikukuu, Ijumaa baada ya saa sita mchana, Jumamosi na Jumapili.