Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imefanya operesheni maalum katika mkoa wa Iringa na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 276 za dawa za kulevya aina heroin na bangi na watu 12 wakihusishwa na dawa hizo.

Akitoa taarifa kwa niaba ya Kamishna Jenerali Agosti 27, 2023 Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka hiyo, Daniel Kasokola, amesema lengo la operesheni hiyo ni kuvunja mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Amesema,”operesheni hizi ni moja ya utekelezaji wa mkakati wa kudhibiti upatikanaji wa dawa
za kulevya (Supply Reduction), hivyo kama Kamishna Jenerali anavyoeleza zitafanyika nchi zima, wote wanaojihusisha na kilimo au biashara hii  hakuna ataukwepa mkono wa sheria.”

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kukabiliana na dawa za kulevya nchini, na kuwataka watanzania waungane katika mapambano hayo kama walivyofanya wananchi wa Kisimiri juu, Lesinoni na Lenglong mkoani Arusha na wale wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kuamua kuondoa mimea ya bangi na mirungi katika maeneo yao.

Akizungumzia operesheni hiyo, Mtendaji wa kata ya Malolo wilaya ya Kilosa, Fredinand Litweka amesema uongozi wa Wilaya umekuwa wakifanya jitihada kadhaa bila mafanikio hivyo, kufika kwa mamlaka katika maeneo yao kumeongeza chachu ya mapambano dhidi ya kilimo na biashara ya dawa za kulevya.

Nao wakazi wa Ruaha Mbuyuni, akiwemo Jefari Jeda wameunga mkono jitihada hizo wakidai dawa za kulevya zina madhara makubwa na kwamba wako tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali.

West Ham kubeba mzigo wa Maguire
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Agosti 28, 2023