Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah Bares amesema atatumia mapumziko ya majuma matatu ya Kalenda ya FIFA kuendelea kukinoa kikosi chake ikiwa ni pamoja na kupata mechi tatu za kirafiki nchini Burundi.

Akizungumza kutoka Kigoma, kocha huyo amesema hiki ni kipindi ambacho anataka kukiweka kikosi chake sawa kwani kina wachezaji wengi wapya na wengine ambao hawajawahi kucheza hata mechi hiyo.

“Wachezaji wetu tumewapa siku tatu tu za mapumziko baada ya hapo watarejea na kuanza programu za mazoezi kwa ajili ya mechi za kirafiki ambazo zitatupa ukomavu kwenye ligi, kama unavyoona timu yetu bado ngeni, ina wachezaji baadhi wapya na wengine hawajabahatika kucheza hata mechi moja ya ligi, tunahitaji kuwapa uzoefu ili wote wawe imara,” amesema.

Amesema mechi tatu tu zinamtosha ili kuweka kikosi chake kwenye hali njema ya mapambano wakati Ligi Kuu itakaporejea.

“Kwangu mimi nahitaji mechi tatu, zinatosha sana, ila nataka zile zenye ushindani na tumeona ndugu zetu wa Burundi timu zao nazo zinajiandaa kwa ajili ya ligi, hivyo wameitikia wito wa kutaka kucheza na sisi mechi za kirafiki, kwa hiyo ningependa kucheza na timu za huko, kama itapatikana nafasi ya wao kuja sawa, lakini sisi wenyewe tunaweza kwenda huko kucheza,” amesema.

Mpaka sasa Mashujaa iliyopanda daraja na kuanza kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, haijapoteza mechi yoyote, ikishinda mechi ya kwanza mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar na suluhu dhidi ya Geita Gold.

Tuhuma zaibua mazito Hispania
Che Malone akaidi amri ya Robertinho