Mara baada ya Maofisa wa Jeshi nchini Gabon hapo jana Agosti 30, 2023 kumpindua Rais wa nchi hiyo Ali Bongo, wamemteua Mwanajeshi mwenzao, Jenerali Brice Nguema kuwa Kiongozi wa mpito wa Taifa hilo.

Wakati Nguema anateuliwa kuwa kiongozi wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Rais aliyepinduliwa amekiri kushikiliwa na wanajeshi hao katika makazi yake, huku familia yake ikitenganishwa naye.

Gabon imekuwa chini ya utawala wa familia ya Bongo kwa zaidi ya miaka 50 ambapo Ali Bongo alikuwa Rais akimfuatia Baba yake mzazi, Omar Bongo ambaye alifariki mwaka 2009.

Uamuzi wa Jenerali Nguema kuongoza nchi hiyo maarufu kwa uzalishaji wa mafuta ulifanywa baada ya wanajeshi hao kupiga kura na anatajwa kuwa mtu jasiri na shupavu ambaye ameliongoza jeshi la nchi hiyo katika misheni mbalimbali na hadi anapata uongozi huo, alikuwa mkuu wa kikosi cha kumlinda Rais.

Maofisa wa Jeshi la Gabon walitangaza Agosti 30, 2023 kuiongoza nchi hiyo katika kituo cha Televisheni cha Taifa hilo, ikiwa ni siku chache tangu Uchaguzi Mkuu ufanyike.

Lakini pia, walitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Jumamosi, ambapo Rais Ali Bongo alitangazwa mshindi, huku Jenerali Nguema akizunguka mitaani nchini humo akiwa amebebwa juu na Wanajeshi wenzake wakimshangilia.

Taifa Stars yaweka kambi Tunis, Tunisia
Ushirikiano silaha kuu ya kuzuia uhalifu - Polisi