Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema anatengeneza timu ambayo kila mmoja atakuwa na uwezo wa kufunga na sio kumtegemea mchezaji mmoja.

Gamondi ambaye timu yake imefunga mabao 10 katika mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya KMC FC na JKT Tanzania, amesema kuwa Young Africans anayoitengeneza kila mmoja atakuwa na uwezo wa kufunga.

Amesema hayo baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex juzi Jumanne (Agosti 29).

Kocha huyo raia wa Argentina alizungumzia mchezo namna ulivyokuwa mgumu kipindi cha kwanza kutokana na aina ya wapinzani wake walivyocheza kwa faulo nyingi na kuzuia na kwamba baada tu ya kupata bao la uongozi dakika ya 45 ilisaidia wachezaji kujiamini.

Amesema kipindi cha pili timu yake ilicheza vizuri na kila mmoja alikuwa akionesha uchu wa kutaka kufunga mabao na hatimaye wakafanikiwa kuondoka na ushindi mkubwa.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amesema mabadiliko ya wachezaji aliyofanya hasa kipindi cha pili yaliwagharimu tofauti na matarajio yeke.

Amesema: “Nilifanya mabadiliko ili wachezaji wakaendelee kuminya mianya ya wachezaji wa Young Africans wasipenye kisha watafute goli kwa akili lakini walijikuta wanafanya makosa na kushindwa kufanıya majukumu yao vizuri.”

Marufuku kutuma nyaraka za Serikali kwa WhatsApp
Rais Mwinyi aahidi kutimiza ahadi kwa Wananchi