Unakumbuka Ditram Nchimbi alicheza mwaka mzima bila kufunga bao katika Ligi Kuu Bara akiwa na Young Africans? Sasa nyota wa Singida Big Stars, Francis Kazadi anaanza kuinyemelea rekodi hiyo kutokana na ukame wa mabao alionao tangu alipojiunga na timu hiyo Januari mwaka huu.

Baada ya kutamba katika Kombe la Mapinduzi 2023 alipoibuka Mfungaji Bora akifunga mabao sita, mambo yameonekana kuwa tofauti kwa Kazadi anayetimiza miezi minane sasa bila kuziona nyavu, akibakisha miezi minne tu ili aifikie rekodi ya Nchimbi.

Katika kipindi cha miezi minane ambayo Kazadi ameitumikia Singida, timu hiyo imecheza mechi 15 za Ligi Kuu zilizoonekana mlima mrefu kwa nyota huyo wa zamani wa AS Vita kuzifumania nyavu.

Mechi hizo ni dhidi ya Kagera Sugar, Azam, Simba SC, Young Africans, Mtibwa, Polisi Tanzania, Ihefu, Coastal Union, KMC, Dodoma Jiji na Namungo FC.

Kiujumla ukame kwa Kazadi haupo katika Ligi Kuu pekee, bali hata mechi za mashindano mengine na zile za kirafiki kwani katika kipindi chote cha miezi minane aliyoitumikia timu hiyo, amefunga bao moja tu katika michezo 22 ambalo alilipata katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Mbeya City ambao Singida iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.

Katika Kombe la Mapinduzi, Kazadi alionekana tishio katika kufumania nyavu jambo lililofanya wengi waamini angekuwa mwiba katika kupachika mabao kwenye Ligi Kuu na ASFC, japo mambo yameenda sivyo.

Mabao sita aliyopachika kwenye Kombe la Mapinduzi yalitosha kumfanya awe mfungaji bora, manne kati ya hayo akifunga katika mechi moja dhidi ya Azam FC.

Kaimu Kocha wa Singida, Mathias Lule amesema ana imani na kiwango cha Kazadi na atafunga tu.

“Kazadi ni mchezaji mzuri na ndio maana tumekuwa tukimpa nafasi na mchango wake kwenye timu ni mkubwa zaidi ya kufunga. Suala la kutofunga linawakuta washambuliaji wengi lakini naamini muda mfupi ujao mtaona.”

Gamondi aiwekea mtego Al Merrikh
Usajili wa Lukaku wamuibua Gaetano Dagostino