Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka amemtembelea Mtoto mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa Msowero Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, anaydaiwa kufanyiwa ukatili na mjomba wake aliyekua akiishi naye kwa kumchoma moto kwenye makalio na mguuni huku mgongoni akiwa na alama za viboko.
Akiwa eneo hilo, Shaka ameagiza kutafutwa kwa walezi hao wa mtoto ambapo awali Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Dumila, Bi. Caroline Makemo alifichua taarifa hizo baada ya kupigiwa simu na ofisa Mtendaji Kata ya Msowero, kwa Lengo kumchukua mtoto na kumlea katika kituo chake cha kulelea watoto yatima.
Caroline amesema, baada ya kufika katika eneo hilo alikuta mtoto akiwa katika hali mbaya huku kidonda kikitoa harufu baada ya kuhoji aliambiwa mjomba wa mtoto amekimbia baada ya tukio hilo na shangazi alikua akimpaka dawa za kienyeji ikiwemo matope jambo limesababisha kidonda kuharibika huku mama mzazi akidaiwa kupata changamoto ya afya ya akili na baba mzazi akiishi mbali na eneo hilo.
Hata hivyo, Daktari aliyempokea mtoto huyo, Yunifa Hezron amesema kwa sasa anaendelea vizuri na ameshapatiwa matibabu ya kuzuia bakteria kusambaa maeneo mengine ya mwili.