Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, limewataka Wafugaji jamii ya Kimasai kuacha kujichukulia sheria mkononi pale wanapokutana na changamoto mbalimbali, hasa za kutuhumiwa kulisha mazao kwenye mashamba ya Wakulima.
Wito huo, umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Alex Mkama katika kijiji cha Maharaka kilichopo Kata ya Doma Wilaya Mvomero wakati wa kikao na baadhi ya wafugaji katika kijiji hicho, huku akiwataka kuwa watulivu wakati kesi yao ya Kujeruhiwa kwa ng’ombe 13 ikifuatiliwa.
“Mnatakiwa kuwa watulivu kwa kipindi hiki ambacho kesi yenu ya kujeruhiwa kwa ng’ombe zenu 13 inaendelea ili mpate haki zenu maana hiki kilichotendeka ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi yetu, watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kwa hatua za kisheria,” alisema kamanda Mkama.
Aidha, Kamanda Mkama aliwataka wafugaji hao kuishi kwa amani na kutojihusisha na migogoro inayoepukika kati yao na Wakulima, kwani migogoro hiyo inaondoa amani na utulivu mara inapotokea katika maeneo yao.