Baada ya Kocha Erik ten Hag kusema kuwa, alimtema Jadon Sancho katika kikosi kilichocheza dhidi ya Arsenal kutokana na kutojituma mazoezini, winga huyo amevunja ukimya akisema amekuwa akitupiwa lawama kwa muda mrefu.

Sancho ametoa kauli hiyo baada ya Ten Hag kusema kuwa, hakumjumuisha nyota huyo katika kikosi hicho kwa sababu hakuwa bora mazoezini.

United juzi Jumapili (Septemba 03) ilikubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu ya England uliochezwa katika Uwanja wa Emirates jijini London.

Sancho hakusafiri na timu hiyo ilipokwenda London kucheza na Arsenal, jambo ambalo lilizuia maswali kutoka kwa mashabiki wa Man United pamoja na waandishi wa habari.

Alipoulizwa Ten Hag kwa nini Sancho sio sehemu ya kikosi hicho, alisema nyota huyo hakufikia levo ambayo ingemfanya ajumuishwe timu.

“Unapaswa kufikia levo kila siku hapa Manchester United na tunaweza kufanya machaguo katika safu ya mbele. Kwa hiyo katika huu mchezo hakuwa amechaguliwa,” alisema.

Hata hivyo, Sancho aliwataka mashabiki wa timu hiyo kutoamini kila ambalo wanalisoma kuhusu yeye.

“Tafadhali usiamini kila kitu ambacho unasoma,” Sancho aliandika katika kurasa zake za mitandao ya kijami.

“Sitoruhusu watu waseme vitu ambavyo sio ya kweli kabisa. Nimekuwa vyema sana katika mazoezi juma hili.”

“Naamini kuna sababu nyingine (kutojumuishwa), ambazo sitaki kuzizungumzia.”

“Nimekuwa mtu wa kutupiwa lawama kwa muda mrefu jambo ambalo sio sawa,” aliandika.

Sancho alisisitiza kuwa ataendelea kupambania nafasi yake katika klabu hiyo na kutoa mchango katika kikosi.

“Naheshimu uamuzi wote unaofanywa na makocha, nacheza na wachezaji wazuri na ninafurahi kucheza nao, kitu ambacho naamini kila wiki ni ushindani,” alisema.

Sancho, 23, alitua Man United mwaka 2021 akitokea Borussia Dortmund kwa dau la Pauni Milioni 73.

Hata hivyo, amekuwa akipata shida kuwa na muendelezo wa kiwango kizuri kama alichokionyesha alipokuwa Dotmund.

Katika michezo 58 aliyoitumikia Man United tangu alipotua, mchezaji huyo amefunga mabao tisa na kutoa pasi sita za mabao.

Wahamiaji zaidi ya 3,000 wapewa uraia wa Tanzania
Ajali: Basi la Ngasere lapata ajali Mpwapwa