Wakati Kikosi chao kikiendelea na maandalizi makali kuelekea mechi ya Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, Uongozi wa klabu hiyo umesema wataitumia michezo yao miwili dhidi ya Wazambia hao kujiandaa dhidi ya Al Ahly kwenye mechi ya African Football League ‘AFL’.

Simba SC ambayo Septemba 16, itakuwa Ugenini nchini Zambia kucheza mechi hiyo ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kurudiana Septemba 29 hapa nchini, ndiyo itakayocheza mechi ya ufunguzi ya michuano ya African Football League katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Ahly.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Salim Abdallah Try Again’, amesema baada ya kujua wapinzani wao wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni Power Dynamos ya Zambia pamoja na Al Ahly katika michuano ya Afrika Football League, Kocha Roberto Oliveira anafanya maandalizi makali.

Try Again amesema dhamira yao ni kushinda mataji ya ndani na kufika hatua ya nusu fainali ya Afrika pamoja na kushindana katika michuano mikubwa ya ‘AFL’.

Amesema benchi la ufundi linaloongozwa na Robertinho, linafanya kazi yake kwa umakini baada ya kumpatia kila kitu ikiwamo usajili wa wachezaji wenye Uwezo na uzoefu mkubwa wa michuano ya Afrika.

“Tumefanya usajili mkubwa sana kupitia dirisha kubwa la usajili mwaka huu na ukweli ni kuwa miongoni mwa sababu kubwa ni ushiriki wetu wa mashindano mbalimbali ikiwamo ya AFL, tumejipanga kushindana katika michuano yote mikubwa kufikia malengo yetu,” amesema Try Again.

Ameongeza kuwa wanauzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa, wanaenda kucheza na Power Dynamos kUsaka ushindi kwa michezo yote miwili na kutinga hatua ya makundi lakini pia kuitumia kama sehemu ya maandalizi dhidi ya Al Ahly.

“Tunatambua Ugumu wa michuano iliyopo mbele yetu na ninaamini Robertinho anaendelea na maandalizi kufikia malengo yetu, kushinda kila mechi iliyopo mbele yetu, hatutaki kwenda kushiriki, tunataka kuwa miongoni mwa timu zinazokwenda kushindana na klabu kubwa ikiwamo Al Ahly na zitakazokuwa mbele yetu,” amesema mwenyekiti huyo.

Luhemeja ataka ubunifu wa kazi wenye malengo
Serikali za Afrika ziwape Wakulima Pembejeo za bei nafuu