Wizara ya Maliasili na Utalii, inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali inayolenga kuendeleza, kukuza na kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo vivutio vilivyopo Kisiwa cha Ukerewe palipo na Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuvifanya vivutio vya Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza kuwa na tija kwa Taifa.
Akijibu swali hilo amesema, “Wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliratibu ziara ya kituo cha Televisheni cha ITV kwenda kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe vikiwemo Mapango ya Handebezya na Jiwe linalocheza kwa ajili ya kuandaa documentary ambayo itakapokamilika itaonyeshwa katika kipindi cha ITV cha Chetu ni Chetu.”
Aidha, amefafanua kuwa Wizara inaendelea kutoa mafunzo kuhusu uanzishwaji wa utalii wa utamaduni ambapo hadi sasa kuna vikundi vya utalii wa utamaduni vikiwemo Ukerewe (Ukerewe cultural tourism Enterprises) na Nansio (Nansio cultural tourism Enterprises).