Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Marais saba kutoka Afrika wamethibitisha kuwa kesho Septemba 7, 2023 watashiriki majadiliano ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula – AGRF, linaloendelea jijini Dar es Salaam.

Msigwa ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya utaratibu utakavyokuwa katika kikao hicho cha marais na kudai kuwa jukwaa hilo, ambalo lilianza Septemba 5, 2023 linatarajiwa kukamilika Septemba 9, 2023 ambapo fursa mbalimbali katika Kilimo zinazopatikana Tanzania zinawekwa wazi kwa washiriki.

“Marais waliothibitisha kushiriki ni saba, Labda na wengine wataendelea kujitokeza kwa sababu mkutano ni kesho, inawezekana wakaongezeka au wakaja kwa uwakilishi,” amesema Msigwa.

Msigwa amesema marais hao watafanya majadiliano, kila mmoja kutoa hotuba yake, kupokea taarifa mbalimbali na badaye maazimio ya mkutano huo yatawasilishwa ambapo jioni wageni wataalikwa Ikulu ambapo tuzo ya mzalishaji wa Chakula Afrika itatolewa ikiwa ni kutambua mchango wa uzalishaji wa chakula Afrika.

“Kabla ya mkutano huo, asubuhi ya kesho Rais Samia Suluhu Hassan asubuhi atahutubia vijana na kupokea taarifa juu ya namna vijana wa Afrika wanajihusisha na kilimo na kutumia fursa mbalimbali za kilimo na baada ya taarifa hiyo na yeye atatoa muelekeo wake juu ya namna anavyoona bara la Afrika linavyoweza kusaidia vijana kupata ajira kupitia kilimo,” amesema Msigwa.

Polisi wa doria wawekwa mtu kati na Walevi
Dkt Mollel: Madaktari Wazalendo 2,469 wamesajiliwa