Manchester United inaongoza kwa matumizi makubwa ya fedha kwenye usajili wa wachezaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita baada ya kutumia Pauni Bilioni 1.19 kuliko kiwango ilichoingiza kwenye mauzo ya wachezaji wake, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya CIES Football Observatory.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Manchester United tangu mwaka 2014 imetumia Pauni takribani Bilioni 1.67 kununua wachezaji wapya na kuingiza karibia Pauni Milioni 481 kwenye mauzo ya wachezaji wao.
Chelsea inashika nafasi ya pili ambapo ilitumia Pauni Milioni 883, wakifuatiwa na matajiri wa Ufaransa klabu ya Paris St-Germain waliotumia Pauni Milioni 863 kununua nyota wapya.
Arsenal waliotumia Pauni Milioni 745 na Manchester City Pauni Milioni 732 wanashika nafasi ya tano na ya sita kila mmoja.
Jumla ya klabu 13 za Ligi Kuu ya England ziko kwenye orodha ya klabu 20 zilizotumia fedha nyingi kununua wachezaji.
Takwimu zilizotumika zinajumuisha ada kamili za uhamisho, ada za wachezaji inaowanunua kwa mkopo na matumizi mengine yanayohusiana na usajili wa wachezaji.
Usajili wa kishindo ni pamoja na ulioweka rekodi ya Ligi Kuu ya England wa kumnunua kiungo Paul Pogba kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 89.5 mwaka 2016, Romelu Lukaku Pauni Milioni 75 mwaka 2017 na Harry Maguire Pauni Milioni 80 mwaka 2019.
Katika nyota hao watatu ni Maguire pekee aliyesalia kwenye kikosi cha Man United huku Lukaku akiuzwa Inter Milan kwa Pauni Milioni 74 mwaka 2019 akiwakilisha mauzo yao makubwa ya mchezaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita huku Pogba akiondoka kama mchezaji huru msimu uliopita baada ya mkataba wake na klabu hiyo kumalizika.