Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali imewekeza katika teknolojia ya kilimo kinachomili mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira inayotekelezwa nchini.
Dkt. Jafo amesema hayo hii leo Septemba 8, 2023 wakati alipokuwa akichangia mjadala wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Septemba 08, 2023.
Aidha, ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kuunga mkono juhudi hizo za Serikali kwa kufadhili miradi ya kilimo inayotekelezwa nchini ili pawepo na tija na uhakika wa chakula.
Kutokana na Makubaliano ya Paris kuhusu nchi zilizoendelea kuchangia fedha kwa mataifa yanayoendelelea katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Waziri Jafo alipendekeza kupitia fedha hizo pia pawe na mafungu
maalumu ya kuwezesha kilimo cha kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Waziri Jafo pia alisema ili kukabiliana na changamoto ya ukame unaosababishwa na uhaba wa mvua katika baadhi ya maeneo Serikali imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya uchimbaji wa malambo 114 ya umwagiliaji.