Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka Madiwani wa Mkoa wa Dodoma kuwa mabalozi wa Usalama na Afya katika miradi yote wanayoisimamia kwenye kata zao, ili kulinda nguvu kazi dhidi ya magonjwa na ajali maeneo ya kazi.

Luhemeja ametoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi, yaliyoandaliwa na OSHA kwa Madiwani wa Viti Maalumu na Wajasiriamali Wanawake wa Mkoa wa Dodoma, yaliyoenda sambamba na zoezi la upimaji Afya wa magonjwa yatokanayo na kazi katika Ofisi za OSHA Dodoma.

Amesema, “Mkoa wa Dodoma unamiradi mingi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya ujenzi, maji, barabara, upanuaji wa mji n.k. kuna haja ya kuweka mifumo dhabiti ya kumlinda mfanyakazi dhidi ya vihatarishi vya magonjwa na Ajali vinavyoweza kutokea wakati wa utekelezaji wa miradi hii,” alisema Luhemeja.

Kwa upande wake Mbunge wa viti Maalumu wa Mkoa wa Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Toufiq amesema mafunzo hayo kwa Madiwani yamekuja muda muafaka, kutokana na wingi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

“Mtakapo rudi katika maeneo yenu mkawe mabalozi wa kuitangaza OSHA, Serikali imetoa fedha nyingi za maendeleo katika mkoa wetu na kuna miradi mingi inatekelezwa ikiwemo Ujenzi wa Barabara, Ujenzi wa Reli SGR, na Bomba la Mafuta na miradi hii inapita kwenye maeneo yetu ni wajibu wetu kusimamia,” amesema Toufiq.

Akizungumza kwa niaba ya madiwani, Mwenyekiti wa Madiwani Mkoa wa Dodoma, Mwanaharusi Bata ameipongeza OSHA kwa kuendesha programu ya Mafunzo hayo huku akiahidi kuwa wataifikisha elimu hiyo ya usalama na afya walioipata katika miradi mbalimbali inayotekeleza kwenye maeneo wanayotoka.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha madiwani kuhusu majukumu mbalimbali ya OSHA, ili wanapopitisha na kusimamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo waweze kushirikiana na OSHA katika kulinda nguvu kazi kwa kuboresha mifumo ya usalama na afya katika miradi hiyo.

“Mafunzo haya ni sehemu ya maelekezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu na tutahakikisha tunaendelea kutoa elimu na kuyafikia makundi mbalimbali na moja wapo ni hili la watunga sera ili inapotokea wanakaa katika mabaraza ya kupitisha miradi basi waangalie miradi hiyo kama imekidhi viwango vya usalama na afya kama sheria husika inavyo elekeza,” amesema Bi. Mwenda.

Matumaini kibao kwa kocha Middendorp
Sergio Ramos: Nilikataa kusaini mkataba PSG