Ligi ya Championship msimu wa 2023/24, inatarajiwa kuanza leo Jumamosi (Septemba 09) kwa timu nane kushuka dimbani katika viwanja vine tofauti.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, inaanza leo Jumamosi (Septemba 09) na kutarajiwa kumalizika Mei 4, mwakani, huku kila timu ikitarajiwa kushuka dimbani katika mizunguko 30.

Timu ya Mbeya City ambayo imeshuka kutoka Ligi Kuu, itafungua msimu mpya kwa kuikaribisha Green Warriors FC, Stand United itakuwa ugenini kupepetana na TMA FC, Mbeya Kwanza itavaana na Polisi Tanzania wakati Pan Africans ikicheza Copco FC ugenini.

Kesho Jumapili (Septemba 10) kutakuwa na michezo mitatu, ambapo Fountain Gate FC itacheza na Ruvu Shooting FC, Transit Camp FC itakuwa ugenini kuvaana na Ken Gold FC huku Mbuni FC ikicheza na Biashara United.

Mzunguko wa kwanza utakamilishwa keshokutwa kwa mchezo mmoja, Pamba FC ikiwa mwenyeji wa Cosmopolitan FC.

Kocha wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi ya msimu mpya, na anaamini mwaka huu watafanya vizuri.

“Nina imani na kikosi changu, kitaanza ligi hii vizuri na nina uhakika tutacheza Ligi Kuu msimu ujao, kikubwa ni ushirikiano kutoka kwa mashabiki wetu,” amesema.

Amesisitiza kuwa mipango mikubwa ya klabu hiyo ni kuhakikisha wanarejea Ligi Kuu, wamefanya maandalizi bora ambayo yanawapa matumaini ya kufikia malengo yao.

Kocha wa Green Warriors FC, Rashid Mussa amesema wamejiandaa, kuhakikisha wanaanza ligi hiyo wakiwa bora, na wapo tayari kuhakikisha wanafikia malengo.

Diwani CCM achoshwa na mabadiliko
Mashabiki Rwanda waisubiri Young Africans