Aliyekuwa Kocha wa timu ya taifa ya Wanawake ya Hispania, Jorge Vilda amesema kuwa hakufanyiwa haki kutimuliwa kazi katika kikosi hicho, kutokana na kupata mafanikio makubwa ya kubeba Kombe la Dunia la Wanawake, huku akidaiwa kuhusika na kashfa inayomkabili Rais wa Shirikisho la Soka Hispania (RFEF), Luis Rubiales.

Vilda hivi karibuni alitimuliwa kazi baada ya kuonekana akitetea tabia ya Rubiales ya kumbusu mchezaji Jenni Hermoso bila ridhaa yake wakati wa sherehe za kukabidhiwa taji zilizofanyikia Sydney, Hispania.

Kocha huyo alionekana kupinga kitendo cha wajumbe wa mkutano wa RFEF walipotaka Rubiales atangaze kujiuzulu wadhifa wake kitu kilichotafsiriwa kuwa na yeye anahusika kwa kutetea maovu ya rais huyo.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), tayari lilishamsimamisha kazi Rubiales kupisha uchunguzi wa sakata lake linalomkabili.

Kocha huyo alisisitiza kuwa maamuzi yaliyofanywa juu yake ni uonevu kwani yeye hahusiki na chochote kuhusu kitendo hicho.

“Katika soka lolote linaweza kumtokea mtu yoyote, lakini mara nyingi matukio ya kufukuzwa huwa yanahusisha zaidi makocha.

“Kimsingi ninaweza kukabiliana na changamoto iliyonitokea lakini sijahusika kwa chochote na hii imefanyika kwangu kitu ambacho ninaona ni uonevu.

“Ni mwaka mzuri kwangu kutokana na rekodi niliyoiweka Hispania kwa kuipatia Kombe la Dunia la Wanawake kwa mara ya kwanza, nimefukuzwa kitu ambacho siyo haki,” alisema.

NFRA yapanga kununua tani 305,000 za Nafaka
Upatikanaji wa Pembejeo nchini kuimarishwa - Majaliwa