Serikali imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambapo hadi kufikia Julai, 2023 umepungua na kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 4.5 ya Julai, 2022, kutokana na jitihada madhubuti na usimamizi ambao utasasaidia kuendelea kupungua na kubaki ndani ya lengo, ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa chakula nchini unazidi kuimarika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge jijini Dodoma na kuongeza kuwa Tanzania imeendelea kuwa na mfumuko wa bei wa chini, ikilinganishwa na nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki – EAC.

Amesema, katika kuhakikisha Serikali inafikia azma ya kutekeleza utoaji wa huduma kwa wananchi na ujenzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati, Serikali imeendelea kuongeza maarifa na matumizi ya teknolojia na mifumo ya TEHAMA kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake mbalimbali.

Aidha, Majaliwa ameongeza kuwa, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali pia ilikusanya shilingi bilioni 26,241.8 sawa na asilimia 93.7 ya lengo, ikilinganishwa na shilingi bilioni 24,396 mwaka 2021/2022.

Kati ya kiasi kilichokusanywa, mapato ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 21,411.4, sawa na asilimia 95.6 ya lengo, makusanyo yasiyo ya kodi yalikuwa shilingi bilioni 3,845.5, sawa na asilimia 83.5 ya lengo na mapato kutoka vyanzo ya halmashauri yalikuwa shilingi bilioni 984.9, sawa na asilimia 97.3 ya lengo.

BFT warudisha salamu za shukurani serikalini
NFRA yapanga kununua tani 305,000 za Nafaka