Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul ameagiza Mahakama na Jeshi la Polisi kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana na shirika la Utu Kwanza kusaidia upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa wafungwa na Mahabusu wasio na uwezo, ili wapate haki.

Gekul ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akifungua dawati la Msaada wa kisheria lililoanzishwa na Shirika lisilo la kiserikali Ia Utu kwanza lililojipanga kutoa huduma ya Msaada wa kisheria katika Mahakama kwa kuanzia Wilaya ya Kinondoni.

Amesema, Mashirika hayo yanatakiwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya watu kwa kuzingatia kipaumbele cha utu kwenye haki jinai na wajibu wa kuwatumikia Watanzania katika kudumisha amani na mshikamano.

“Kupitia muhimili wa Mahakama na sisi tutalisukuma ili ione namna ya kuridhia kuanza kwa dawati hilo bila kuathiri shughuli za kimahakama, ni matarajio yetu shirika litaendelwa kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria,” alisema Gekul.

Naye Mkurugenzi wa Utu kwanza, Wakili Shehzada Walli, amesema lengo la kuanzisha shirika hilo ni kusaidia wafungwa na kwamba dawati la kutoa msaada wa kisheria litasaidia watu wanaofikishwa Polisi wasio msaada wa kuweza kuwajulisha ndugu na yeyote kuhusiana na kile kinachoendelea.

Kwa upande, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mansoor Altaf Hiran alisema kuwepo kwa dawati hilo ni jambo la muhimu kwani itasaidia wananchi kupata hali zao na kwamba kila mtu akipata haki yake amani itakuwepo.

Aidha, Inpekta Msafiri Kundi kutoka Gereza la Keko alisema dawati hilo likianza litakuwa na msaada kwa wafungwa na mahabusu kwani wapo baadhi yao hawana uwezo wa kupata Mawakili.

Idadi vifo vya Tetemeko Morocco yazidi Watu 2,000
Ahmed Ally: Tunataka heshima yetu idumu