Jumuiya ya Watanzania waishio Guangzhou Nchini China – Diaspora imeahidi kushirikiana na Balozi mpya wa Tanzania nchini humo, Khamis Mussa Omar wakisema wanaamini misingi iliyojenga na Balozi anayemaliza muda wake, Mbelwa Kairuki imerithiwa na Maofisa aliowaacha ofisini ambayo itakua Dira elekezi ya kukamilisha mafanikio ya umoja wao.
Kupitia risala waliyoisoma katika hafla ya kumuaga Balozi Mbelwa Kairuki jijini Guangzhou, Diaspora hao wamesema watamkumbuka kwa mambo mengi ikiwemo jitihada zake zilizopelekea mahusiano mema kati yao na Biashara kati ya Tanzania na China kuongezeka maradufu.
Wamesema, “kabla yako (Balozi Kairuki), tuliona ofisi ya balozi kama kambi ya jeshi, lakini ukarimu wako umetufanya kuiona balozi kama ilivyo milango ya maabadi kwa waumini wanapotaka kushukuru ama kumlilia shida Mola wao. Hukuwahi kubweteka na cheo hadi mjasiriamali wakawaida ana namba yako na umekua swahiba kwa lugha za kileo.”
“Watanzania wengi wanaoishi hapa walilazimika kusafiri umbali wa saa 8 kwa treni kwenda Beijing kufuata huduma mbalimbali za kibalozi. Ulituahidi kufuatilia jambo hili na hatimaye Ubalozi Mdogo umefunguliwa na sasa watanzania tunaoishi hapa Guangzhou na hatutaabiki tena,” wamesema.
Diaspora hao wameongeza kuwa, “zamani makampuni yaliyokuwa yanauza bidhaa yalikuwa ni machache sana tena ni ya wachina. Leo hii Makampuni zaidi ya 100 ya Watanzania yamesajiliwa hapa China kuuza Mahaage ya Soya, Ufuta, Kahawa, Korosho, bidhaa za baharini. Haya ni matokeo ya uhamasishaji wako.”
Hata hivyo, wamzidi kubainisha kuwa dhamira yao si kumsifu na kumvika kilemba cha ukoka Balozi Mbelwa, lakini
anastahili heshima, pongezi na sifa kwa kulitendea haki Taifa, kuwaheshimisha na kwamba wanaamini mema yote aliyoyafanya yataendelezwa na Balozi Khamis Mussa Omar.