Taarifa zinaeleza kuwa kuna uwezekano beki wa kulia kutoka nchini DR Congo Djuma Shabani akasajiliwa Azam FC, wakati wa Dirisha Dogo la Usajili mwezi Januari 2024.

Mpango huo unatajwa kuwa katika hatua nzuri kufuatia Beki huyo kuachana na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara na mwishoni mwa juma lililopita alionekana akiitumikia Azam FC katika mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Arta Solar ya Djibouti ambayo ilikubali kichapo cha 2-1 katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Hata hivyo imefahamika kuwa jukumu la kuongezwa kwa Djuma Shabani limeachwa kwa Kocha Mkuu Youssouph Dabo ili kumsoma kwa sasa ndani ya kikosi hicho na kuchagua mchezaji gani wa kumchomoa ili beki huyo Mkongomani achukue nafasi kulingana na kanuni.

Kanuni za usajili kwa mapro wa kigeni zinataka klabu isizidishe idadi ya wachezaji 12 na tayari Azam imeshakamilisha, hivyo ili Djuma aingie ni lazima ipunguze mmoja wa nyota waliopo sasa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarimn Amin Popat’ amesema suala la usajili wa beki huyo lipo mkononi mwa kocha Dabo.

Djuma Shabani akiwa na baadhi ya wachezaji wa Azam FC kwenye mazoezi ya timu hiyo jijini Dar es salaam.

Popat amesema hawana shaka na kiwango cha nyota huyo ila suala la usajili wake wamemuachia Dabo japo itawalazimu kupunguza wengine ili aingie.

“Tuna wachezaji 12 wa kigeni kama kanuni inavyohitaji sasa endapo kocha ataona anamfaa katika timu basi tutamsajili huku pia suala la kuchagua wa kumpisha tutamuachia atoe uamuzi,” amesema.

Wakati Popat akizungumza hayo, imefahamika kuwa mastaa waliokalia kuti kavu ni Mlinda Lango Ali Ahamada aliyetakiwa kumpisha Djuma ila aligoma baada ya kudai viongozi walichelewa kumpa taarifa hizo.

Mbali na Ahamada, Mlinda Lango mwingine Mghana Abdulai lddrisu huenda pia akaachwa kutokana na kile kinachoelezwa kutokuwa kwenye maelewano mazuri na kocha wake wa makipa, Khalifa Ababakar Fall.

Endapo lddrisu ataachwa itatoa nafasi kwa Mlinda Lango Mnigeria John Noble anayekipiga kikosi cha Kitayosce kusajiliwa kwani viongozi wa timu zote mbili wamewasiliana juu ya upatikanaji wake.

Matapeli Ramli chonganishi wakalia kuti kavu
Rais azindua mradi kuimarisha uchumi wa Kilimo