Beki wa FC Barcelona, Inigo Martinez amesisitiza kwamba wana uwezo wa kubeba ubingwa wa Ligi Mabingwa Ulaya msimu huu.

Mchezaji huyo aliyesajiliwa katika dirisha la majira ya kiangazi akitokea Atheltic Bilbao, anaamini chini ya kocha Xavi Hernandez watafanya mambo makubwa baada ya kubeba ubingwa wa La Liga msimu uliopita.

Akizungumza kuhusu ndoto yao kubwa msimu huu, beki huyo alisema: “Kweli, siwezi kuzungumza mengi kuhusu Ligi Mabingwa Ulaya, lakini tumejiandaa kuelekea mechi zetu za makundi. Michuano itakapofika kocha atatuambia cha kufanya. Kushindana na kupata matokeo mazuri ndio malengo yetu makubwa.

“Licha ya mabadiliko makubwa kwenye kikosi tumeona timu imesheheni wachezaji wengi vijana. Tunajua ushindani utakuwa mkubwa. Tuna kikosi kipana, hivyo tutapambana hadi mwisho kwa sababu tunataka kushinda mataji yote.”

Xavi aliweka rekodi ya kuipa Barcelona ubingwa wa LaLiga msimu uliopita na kutokana na usajili waliofanya dirisha la usajili la kiangazi, beki huyo anaamini wanaweza kuleta ushindani kwa wapinzani wao, hususan Real Madrid ambayo ilibeba Copa del Rey.

Mara ya mwisho Barcelona kubeba ubingwa wa Uefa ilikuwa 2015 kabla ya Lionel Messi kuondoka. Miamba hiyo ya Catalunya iliichapa Juventus kwa mabao 3-1 kwenye fainali iliyochezwa Berlin nchini Ujerumani na kubeba ubingwa kwa mara ya tano. Kikosi cha Barcelona kipindi hicho kiliundwa na Ivan Rakitic, Neymar na Luis Suarez.

Katika mchezo huo Alvaro Morata alisawazisha bao matokeo yakawa l-l, lakini Suarez na Neymar walifunga mabao mawili kwa Barcelona na kutoboa kwenye fainali.

Messi na Neymar waliibuka kuwa wafungaji bora kwenye michuano hiyo wakiwa na mabao 10 kila mmoja sambamba na Cristiano Ronaldo. Barcelona ilimaliza kundi Fmbele ya Paris Saint-Germain, Ajax na APOEL kabla ya kuziondoa Manchester City, PSG na Bayern raundi ya mtoano.

Singida Fountain Gate yabisha hodi Ikulu
Namungo FC yasisitiza kupambana