Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’, Walace Karia amesema wamedhamiria kuvuka zaidi ya hatua ya makundi wakati Taifa Stars itakaposhiriki Fainali za Mataifa ya Afrika, nchini Ivory Coast mwakani.

Taifa Stars ilifuzu kwa Fainali hizo baada ya kutoka sare ya bila kufungana Septemba 7, mchezo uliochezwa Annaba, nchini Algeria.

Stars ilishika nafasi ya pili kwenye kundi lake nyuma ya Algeria na kuziacha Uganda yenye pointi saba na Niger iliyomaliza ya mwisho ikiwa na pointi nne.

Hii ni mara ya tatu Taifa Stars inafuzu Fainali hizo ambapo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1980 Lagos, Nigeria na ya pili mwaka 2019 Cairo, Misri.

Karia amesema wameweka malengo ya Taifa Stars kwenda mbele zaidi ya hatua ya makundi kwenye fainali hizo zitakazofanyika Ivory Coast, mwakani.

“Ukijikubali wewe ni mkubwa basi utakuwa mkubwa na safari hii tunataka Taifa Stars inapokwenda AFCON 2023, Ivory Coast isiishie hatua ya makundi,” amesema Karia.

Karia amesema wanataka kuifanya Tanzania kuwa taifa kubwa kwenye mchezo wa soka katika Bara la Afrika.

Katika hatua nyingine Karia amewatakia heri wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Young Africans na Simba SC.

Young Africans na Simba SC zitakuwa Rwanda na Zambia kucheza mechi zao za raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh na Power Dynamos kesho Jumamosi (Septemba 16).

MSISITIZO: Klopp aikataa mazima Ujerumani
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 15, 2023