Serikali Nchini, imewataka wasimamizi wa sheria katika maeneo ya Viwanja vya Ndege na Bandarini kuendelea na usimamizi na udhibiti wa kemikali, zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.

Rai hiyo, imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Mitawi wakati akifungua warsha kwa Maafisa wa serikali waliopo katika bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.

Amesema, Maafisa forodha na wasimamizi wa Sheria katika maeneo ya mipaka wana wajibu mkubwa wa kusimamia uingizaji wa bidhaa mbalimbali zinazoingizwa nchini zikiwemo kemikali ambazo zimekuwa zikileta madhara mbalimbali katika jamii yakiwemo magonjwa ya saratani ya ngozi, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Abdallah Mitawi katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya itifaki ya montreal iliyofanyika Septemba 15, 2023 Jijini Dar es Salaam.

“Warsha hii ni muhimu kwenu na hii ni kutokana na majukumu yenu ya kila siku…. Naamini mtajenga uelewa mkubwa zaidi katika masuala ya Tabaka la Ozoni na hatimaye kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya Ozoni kwa wengine ili sote kwa pamoja tuongeze juhudi za kuhifadhi Tabaka la Ozoni” amesema Mitawi.

Kwa mujibu wa Mitawi, amesema Maafisa wa Serikali na wasimamizi wa Sheria waliopo maeneo ya mipaka ni wadau muhimu katika udhibiti wa uingizaji wa bidhaa na kemikali zenye ukomo wa matumizi katika jamii na hivyo wana nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi aina ya vifaa vinavyopaswa kutumika.

Dkt. Mwinyi aelezea umuhimu wa Sayansi kwa nchi zinazoendelea
Kagame, Tshisekedi waendeleza malumbano