Kiungo wa Simba SC, Clatous Chama, anaamini mchezo unaofuata wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union utakuwa sehemu ya kusahihisha makosa yao kuelekea mechi ya Mkondo wa Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia, Oktoba Mosi, mwaka huu.

Chama ndiye aliyeisawazishia Simba SC mabao yote mawili katika sare ya 2-2, ikitokea nyuma dhidi ya Power Dynamos juzi Jumamosi (Septemba 16) katika Uwanja wa Levy Mwanawasa nchini Zambia.

Chama amesema kabla ya kuwaza mechi ya marudiano hapo kati kuna mchezo wa ligi, watakaporejea wataanza maandalizi ya mechi hiyo ya Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union kabla ya kurudiana na Power Dynamos.

“Hapa kati kuna mechi ya ligi, akili na nguvu tunaelekeza kwenye mchezo huo, tukimaliza mechi hiyo tunaingia katika maandalizi ya kupambana kwa ajili ya kusaka ushindi na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Ninaimani Dar es Salaam tutapambana zaidi, katika mpira chochote kinaweza kutokea sare ilikuwa si lengo letu, tunaenda kupambana katika mechi ya marudiano,” amesema Chama.

Ameongeza kuwa mechi ilikuwa ngumu na wachezaji walipambana kuhakikisha wanasawazisha lakini Power Dynamos walibadilika tofauti na walivyocheza awali kwenye mechi ya Tamasha la Simba Day, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Chama amesema baada ya kufungwa bao la kwanza walifanikiwa kujiandaa kiakili na kimwili kwa kupeana ishara ya kupambana hadi hatua ya mwisho kusawazisha mabao.

“Muhimu sana kucheza kwa mahitaji ya timu, kocha na kuwapa furaha mashabiki wetu ambao wamekuwa pamoja na sisi katika kila hatua, hatuwezi kuwaambia kwa maneno bali kuhakikisha tunawafurahisha kwa matokeo mazuri uwanjani,” amesema Chama.

Jurgen Klopp: Ilikuwa nafuu kwa Mac Allister
Serikali kushirikisha Vyombo vya Habari uhifadhi Mazingira