Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamaondi amefichua siri ya safu yake ya ulinzi kuwa imara na yenye maelewano uwanjani huku mwenyewe akisema anaendelea kuisuka ili iwe imara zaidi.

Gamondi amesema wachezaji wake wote wanafanya vizuri na anajivunia kuwa nao kikosini lakini kubwa zaidi akaeleza namna mabeki wake wa kati walivyo na ushirikiano na maelewano ndani na nje ya uwanja.

Mabeki wa kati wa Young Africans ni Dickson Job, Bakari Mwanmyeto, Ibrahim Bacca, Gift Fred na ‘bwana mdogo’ Shaibu Mtita aliyepandishwa kutoka timu ya vijana lakini mara nyingi wamekuwa wakicheza Job, Bacca na Mwamnyeto kwa kupokezana jambo ambalo Gamondi amelitolea ufafanuzi.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anafurahishwa na namna mabeki hao wanavyoishi na kuweka wazi kuna muda anawashirikisha katika kuwapanga na kuwapa nafasi ya kutoa maoni na kupendekeza nani acheze kati yao.

“Mabeki wetu wa kati wana ubora mkubwa na kila siku tunajitahidi kujenga safu imara zaidi, nafurahia kuwa nao na mara nyingi tunajadili namna ya kucheza na kuamua tuingie vipi kwenye mechi,” amesema Gamondi akielezea safu yake ya ulinzi ambayo katika mechi saba za kimashindano ilizocheza hadi sasa imeruhusu bao moja tu na kuongeza;

“Sio hao tu, bali kikosi kizima, tunafanya mambo kwa ushirikiano wa karibu ndio maana mnaona matokeo chanya ndani ya uwanja.”

Aidha Gamond amezungumzia nafasi za Gift Fred na Mshambuliaji Hafiz Konkoni, kikosini na kusema muda wao upo na watacheza.

“Ni wachezaji wazuri, tuna mipango nao ndio maana wako hapa, tunajenga timu moja, hivyo kila mchezaji lazima ashiriki na nafasi zao zipo, mtawaona wakicheza,” amesema kocha huyo anayependelea soka la kasi.

Kikosi cha Young Africans leo kimerejea mazoezini kuendelea kujiandaa na mechi zijazo ikiwemo ya kesho dhidi ya Namungo itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni muendelezo wa Ligi Kuu.

Ufalme wa Aishi Manula kurejea Msimbazi
Kocha Ihefu awatupia lawama mabeki