Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amesema kitendo cha kuumia kwa beki wa timu hiyo, Abdallah Kheri ‘Sebo’ ni pigo kubwa ingawa pia ni nafasi kwa wachezaji wengine kupigania namba katika kikosi cha kwanza.

Nyota huyo atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu akipatiwa matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti la kulia juzi katika Hospitali ya Vincent Palloti jijini Cape Town, Afrika Kusini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dabo amesema ni pengo kubwa kumkosa nyota huyo, lakini kama benchi la ufundi wanaamini kila mchezaji aliyepo anaweza kuziba nafasi yake japokuwa kila mmoja ana umuhimu wake.

Daktari wa timu hiyo, Mwanandi Mwankemwa amesema Sebo aliumia gegedu (cartilage) ya maungio ambayo imelika na mifupa midogo midogo kutokana na mlalo wa goti lake la kulia na tege alilokuwa nalo.

“Sebo amefanyiwa upasuaji wa kisasa unaoitwa arthroscopic ambao wametoa mifupa midogo midogo iliyokuwa pia imevunjika na kupandikiza gegedu nyingine. Ameelekezwa mazoezi ya kufanya kwa muda wa mwezi mzima.” amesema Dk Mwankemwa.

Nyota huyo alipata majeraha hayo kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons ambapo timu hiyo ilishinda kwa mabao 3-1 hivyo kutolewa wakati wa mapumziko na nafasi yake ikachukuliwa na beki Nathan Chilambo.

Kabla ya kutua Azam FC, Sebo aliwahi kuchezea JKU, Zimamoto na Ndanda FC.

Thomas Tuchel kuishuhudia Man Utd jukwaani
La Liga kuishusha rungu la adhabu